Duration 5:32

Tazama Ziara ya Waziri wa Ulinzi na JKT Dkt. Stergomena Tax Makao Makuu ya Jeshi Dodoma

83 971 watched
0
274
Published 29 Sep 2021

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax amefanya ziara ya Kutembelea Makao Makuu ya Jeshi yaliyopo eneo la Msalato jijini Dodoma tarehe 27 Septemba, 2021. Mara baada ya kuwasili Makao Makuu hayo alipokelewa mbele ya Jengo Kuu na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo aliyeambatana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule pamoja na Wakuu wa Kamandi za JWTZ, Wakuu wa Matawi na baadhi ya Wakurugenzi kutoka Makao Makuu ya Jeshi. Mheshimiwa Waziri ametembelea Makao Makuu ya Jeshi, ikiwa ni mwanzo wa ziara zake atakazozifanya za kutembelea Kamandi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Brigedi, vikosi, vyuo pamoja na shule kwa lengo la kujitambulisha, kujionea utayari kiutendaji, miundo pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo kiutendaji katika kulinda mipaka ya nchi yetu. Akiwa Makao Makuu ya Jeshi alisomewa Taarifa fupi ya JWTZ kuhusu Dira, Dhima, Muundo, Majukumu ya msingi ya JWTZ, Changamoto kabla ya kuongea na Wakuu wa Kamandi, Wakuu wa Matawi, Wakurugenzi, Maafisa Majenerali, Maafisa Wakuu, Maafisa wadogo pamoja na Askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi. Akiongea mara baada ya kupewa taarifa hiyo, Mheshimiwa Waziri ameahidi kuwa atajitahidi kuzijua changamoto licha ya yeye kuwa mtu wa sera, lakini atafanya kila awezalo kuzitatua cha msingi ni kuwepo kwa ushirikiano na utaalamu katika kuzitatua changamoto hizo. ‘Ni imani yangu kuwa nitajitahidi kuzijua changamoto zote ikiwa ni pamoja na kuzitatua licha ya kuwa mimi ni mtu wa sera. Ili kufanikisha hilo ushirikiano na utaalamu vinahitajika’, alisema. Aidha, alimshukuru Mkuu wa Majeshi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata baada ya kuwasili hapo Makao Makuu. Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na Mheshimiwa Waziri tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 12 Septemba, 2021 na kisha kuapishwa rasmi tarehe 13 Septemba, 2021.

Category

Show more

Comments - 61